Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Arafi, mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi na Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akiwa katika ziara yake nchini Bosnia, amekutana na kufanya mazungumzo na Nedžad Grabus, Rais mpya wa Baraza la Ulamaa wa Jumuiya ya Kiislamu ya Bosnia na Herzegovina. Katika mazungumzo hayo, Ayatullah Arafi alimpongeza Nedžad Grabus na kumtakia mafanikio katika kutekeleza majukumu yake mapya.
Ayatullah Arafi ameeleza kuwa ushiriki wake katika hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Baraza la Ulamaa wa Bosnia na Herzegovina ni ishara ya umuhimu na nafasi ya pekee ambayo viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanaipa Jumuiya ya Waislamu wa nchi hiyo. Aidha, amesisitiza dhamira ya Iran ya kuendelea kuiunga mkono Jumuiya ya Kiislamu ya Bosnia na Herzegovina katika kipindi kipya cha uongozi.
Mjumbe huyo wa Baraza la Walinzi wa Katiba, akizungumzia mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba Bosnia na Herzegovina ni sehemu ya mwili wa Umma wa Kiislamu, amesisitiza kuwa umoja baina ya madhehebu ya Kiislamu ni jambo la lazima. Pia, ameelezea matumaini yake kuwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili utaendelea kama ilivyokuwa hapo awali.
Ayatullah Arafi, akikumbusha kuhusu uungwaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa azimio la Umoja wa Mataifa la kuadhimisha kumbukumbu ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya Srebrenica, amesema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia msingi wa udugu wa Kiislamu, kama ilivyokuwa hapo awali, inajiona kuwa na wajibu wa kuwaunga mkono Waislamu na watu wanaodhulumiwa duniani. Iran imeonyesha wazi dhamira hii, hususan katika miaka ya hivi karibuni, kupitia kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na Ghaza.”
Kwa upande wake, Nedžad Grabus, Rais mpya wa Baraza la Ulamaa wa Jumuiya ya Kiislamu ya Bosnia na Herzegovina, ameushukuru ujumbe wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kushiriki katika hafla ya kuapishwa kwake. Pia, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wenye tija na taasisi za kidini na kielimu za Iran.
Katika mkutano huo pia walihudhuria Abu Dhar Ebrahimi Torkaman, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Bosnia na Herzegovina; Adhem Bičakčić, Mwenyekiti wa Baraza la Jumuiya ya Kiislamu ya Bosnia na Herzegovina; Hussein Efendi Kavazović, Rais wa zamani wa Baraza la Ulamaa wa Bosnia na Herzegovina; Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Mofid Hosseini Kuhsari, Naibu Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Hawza nchini Iran; pamoja na Dkt. Hamid Makarem Shirazi, Mkuu wa Ofisi ya Uwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje katika Mkoa wa Qom.
Maoni yako